SABABU ZA MARCO VERRATI KUKUBALIKA BARCELONA



INGAWA Klabu ya Barcelona kwa sasa imeelekeza nguvu zake kubwa katika soko la usajili kusaka beki wa kulia, pia wanahitaji kuwa na mchezaji mzoefu atakayeingia kikosi cha kwanza na kuwa mwarobaini wa tatizo lao la safu ya kiungo.

Kama inavyojulikana, tatizo kubwa lililoisumbua Barca msimu uliopita ni eneo la kiungo.
Wachezaji wao, ambao waliwategemea katika eneo hilo ni Andres Iniesta, ambaye alikumbwa na majeraha kila kukicha, Ivan Rakitic aliyekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka na Andre Gomes, Denis Suarez walioshindwa kuendana na tamaduni ya klabu hiyo.

Imeonekana kwamba, mtu anayeweza kutatua matatizo hayo ya Wakatalunya hao ni Marco Verratti, mchezaji anayeongoza kwenye orodha ya mastaa wanaosakwa na mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Robert Fernandez.

Kwanza, Verratti amepata bahati ya kukubalika na Klabu ya Barcelona kwa sababu mbalimbali.
Ubora wake ni wa uhakika, kiungo fundi anayejua kutimiza majukumu yake kwa umakini na ameshatabiriwa kuwa ni mchezaji wa kiwango cha hali ya juu, licha ya kwamba ndiyo kwanza ana umri wa miaka 24.

Verratti alianza kuonekana katika soka la ushindani wa kweli alipofikisha miaka 20, na tangu hapo timu kubwa mbalimbali zilianza kumfukuzia.
Ana uwezo mkubwa wa kucheza eneo lolote la safu ya kiungo katika mfumo wa 4-3-3, mfumo ambao Barca walianza kuutumia tangu mwaka 2003.

Alipokuwa akiichezea klabu yake ya zamani ya Pescara, Verratti alionekana kuwa ni kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira akiwa katikati mwa dimba, licha ya umbo lake fupi, na alikuwa na uwezo pia wa kuanzisha mashambulizi ya kasi katika kikosi hicho kilichokuwa kinanolewa na kocha aliyeamini soka la mashambulizi kuliko kukaba kama ilivyo tamaduni ya Italia, Zdenek Zeman.

Hivyo ni vitu vichache, lakini vya msingi ambavyo vimetufungua macho ni kwanini Barca inamfukuzia.
Kwa sasa klabu yake ya PSG ipo kwenye hali ya tahadhari sana. Kuna dalili kwamba timu hiyo itaelekea kwenye anguko.

Hilo linachangiwa na changamoto kubwa ya kutofanya vyema kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mwaka huu pia walijikuta wakilitema taji la Ligue 1 kwa vijana wenye njaa wa Monaco.

Mastaa wengine wa klabu hiyo kwa sasa umri unaelekea kuwatupa mkono, kama vile Thiago Silva, Thiago Motta na Edinson Cavani na kama hiyo haitoshi, mtu aliyekuwa kama chanzo kikuu cha mataji, Zlatan Ibrahimovic, akiwaacha mwaka jana.

Verratti huenda akawa staa wao mwingine mkubwa watakayempoteza, lakini si kwa timu pinzani ndani ya ligi yao wenyewe.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment