HAIJULIKANI Mapango ya Amboni yaligunduliwa lini,taarifa  zilizopo ni kwamba watu wa makabila yaliyoishi jirani na eneo hilo, Wadigo,Wasambaa,Wabondei na Wasegeju,walikuwa wakiyatumia kwa ajili ya matambiko ya mizimu tangu Karne ya 16.
Eneo la Mapango hayo wakati huo lilijulikana kwa jina la Mzimu wa Mabavu,Watu kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi,hufika mapangoni hapo kwa ajili ya kuomba au kutambika.
Kampuni ya Amboni Limited,iliyokuwa ikimiliki mashamba ya Mkonge katika mkoa wa Tanga,ilimiliki eneo hilo la mapango mwaka 1892,ili kulitumia kama sehemu ya kupumzikia.
Serikali ya Tanzania ilianza kutangaza eneo la mapango hayo kuwa eneo la hifadhi mwaka 1922,baada kujlishwa mapango hayo na wamiliki wa Amboni Limited.
Mwaka 1937 Serikali ilipitisha Sheria ya mambo ya kale (Monuments preservation ordinance of 1937) iliyofuatiwa na ile ya mwaka 1953 ambayo imesaidia kulinda mambo ya kale.
Mapango hayo yalitokana na  mabadiliko ya nguvu za asili,zilizobadilisha maumbile ya miamba ya chokaa kipindi cha Jurasiki (Jurassic period) miaka milioni 150 iliyopita.
Kulingana na utafiti uliofanywa, eneo hilo la Mapango,lilikuwa chini ya maji miaka milioni 20 iliyota, na linakadiriwa kuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 234,lenye  mazingira ya uoto wa asili.
NJIA ZILIZOSABABISHA MAPANGO
Utafiti uliofanywa Mturi (1975) njia ya kwanza ni ya maji ya Mvua yanapochanganyika na hewa ya “Carbondioxide” katika anga na kutengeneza tindikali ya kaboni (Carbonic acid) ambayo inauwezo wa kuyeyusha madini ya Calcium Carbonate yanayounda sehemu kubwa ya miamba ya chokaa.
Maji hayo yenye tindikali husababisha mabadiliko yanapoteremka kuelekea aridhini,yafikapo aridhini meza ya maji (Water Table) na yakiendelea kuongezeka,maji hayo yenye tindikali huwa na uwezo wa kuyeyusha maungio ya miamba,na sehemu laini zaidi za miamba na kusababisha nyufa.
Nyufa hizo huzidi kupanuliwa na maji yanayotembea na kusababisha baadhi ya  mawe kuporomoka na kufanya mapango.
Kasi ya maji inapozidi njia ndogondogo hupanuliwa na kuwa kubwa zaidi,na inawezekana mapango madogo madogo kuunganishwa na hatimaye kuwa na mfululizo wa mapango kama yanavyoonekana.
  • MLANGO wa kuingilia katika Mapango ya Amboni,Mlango huo wenye umbo la Bara la Afrika,ni moja ya vivutio vya Mapango hayo.


MWAMBA unaokua na kuongezeka hasa katika kipindi cha Mvua,kutokana na mabadiliko ya kikemikali katika miamba ya Chokaa,inaongezeka kwa kiasi cha milimeta 7 katika kila miaka 100.
MWAMBA wenye Picha Mnyama Chui,iliyopo ndani ya Mapango ya Amboni.
PICHA ya Unyayo amboyo ipo juu ya mapango ya Amboni,umbali wa mita 25.
NJIA nyembamba iliyopo ndani ya Mapango,Watu wenye unene kupita kiasi hushindwa kupita njia hii.
MWAMBA unaoonyesha Matiti wa mwanamke,ambao ni miongoni mwa vivutio vya watalii wa ndani na nje ya nchi.
MWAMBA wenye Picha ya Mamba ambayo inamuonyesha mnyama huyo akiogele ndani ya mapango.
BAO la kete ambalo lipo umbali wa futi 15 kwenda juu ya pango,ambapo watalii wengi huvutiwa na sehemu hii,ambapo Baba wa Taifa alikuwa shabiki mkubwa wa mchezo wa bao.
KOCHI (Sofa) la jiwe ambalo limo ndani ya Mapango ya Amboni,Hamza Ngare (29) akipumzika katika Sofa hilo ambalo lipo katika kituo namba nne (4) kilichopo ndani ya mapango.
WATALII wa ndani ya nchi Seif Amry (kushoto) na Hamza Ngare (kulia) wakitoka nje ya Mapango ya Amboni,baada kujionea vitu vingi ndani ya Mapango hayo.